Serikali imejitolea kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa katika sehemu zote za nchi, huku ikilenga kuinua maeneo ambayo hapo awali yalitengwa.
Akizungumza leo Alhamisi alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo katika kaunti ya Kilifi, Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki alisema serikali ya Kenya Kwanza haitalegeza kamba katika kukamilisha miradi yote iliyoanzishwa, aliwahimiza wakenya kutumia fursa zinazotokana na miradi hiyo kujiwezesha kijamii na kiuchumi.
Katika kaunti ya Kwale, Kindiki alisema serikali inatekeleza ujenzi wa barabara ya kilomita 385 kwa kitita cha shilingi bilioni 25, ujenzi wa nyumba za bei nafuu, Masoko ya kisasa na mabweni ya wanafunzi kwa shilingi bilioni 22.
Kuhusu umeme, Naibu huyo wa Rais alisema shilingi bilioni 2.1 zitatumiwa kuweka umeme kwa nyumba 23,589, biashara na vifaa vingine vya umma.
“Wakazi 650,000 kati ya 1,453,000 wa Kilifi wamejiunga na Taifa Care, mpango wa Afya ambao umewasajili wakenya milioni 30.5 kote nchini,” alisema Kindiki.