Shule za Upper Hill, Musingu zatawazwa mabingwa wa kitaifa

radiotaifa
2 Min Read

Mabingwa wa mchezo wa raga ya wachezaji 15 kila upande baina ya shule za upili wa mwaka wa 2018 -Upper Hill, kutoka Nairobi na vipusa wa Kinale kutoka eneo la kati mwa nchi, wametawazwa mabingwa wapya wa kitaifa.

Upper Hill na Kinale zilisajili ushindi  mjini Kisumu siku ya  jumamosi baada ya kuwalemea mabingwa watetezi wa Afrika mashariki- Kisii ( Nyanza) na vidosho wa St.Joseph ( bonde la Ufa) alama 15 kwa 8 na 23 kwa 5  mtawalia katika fainali.

Nafasi za tatu zilinyakuliwa na wavulana wa Yala walipowalaza washikilizi wa rekodi ya taji hilo mara nane na washindi wa mwaka wa 2019 -Kakamega alama 21 kwa 5 nao mabinti wa Mwira wakawaadhibu Mbagathi alama 19 kwa 12 mtawalia.

Kwenye  Handiboli, wavulana wa Musingu kutoka eneo la Magharibi waliwapiku St. Joseph ya bonde la Ufa alama 30 kwa 19.

Katika Magongo, miamba St. Antony ilinyakua tena taji hilo baada ya kulikosa miaka kadhaa ilipoikwatua FSK Kamusinga magoli manne kwa moja ya mikwaju ya penati kufuatia sare ya bao moja kwa moja.

Warembo wao wa bonde la Ufa – Joseph, hawakuachwa nyuma walipowarambisha sakafu wenyeji Nyamira magoli mawili kwa moja ya matuta baada ya sare katika muda wa kawaida.

Kufuatia ushindi huo, shule hizo zitashiriki kipute cha kila mwaka cha Afrika Mashariki baina ya shule za upili mjini Morogoro nchini Tanzania baada ya muhula wa pili.

Taarifa yake Boniface Musotsi

Share This Article