Murkomen: Waliomshambulia Seneta Osotsi watashtakiwa

Murkomen ametoa wito kwa wanasiasa kuvumiliana, kuepuka ghasia na vitendo vya uhuni.

Tom Mathinji
1 Min Read

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amelaani vikali shambulizi dhidi ya Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi Jijini Kisumu.

Murkomen ametoa wito kwa wanasiasa kuvumiliana, kuepuka ghasia na vitendo vya uhuni.

“Tunalaani vikali shambulizi dhidi ya Seneta Osotsi Jijini  Kisumu. Kisa hicho hakikubaliki kamwe,” alisema  Murkomen.

Waziri huyo alitoa wito kwa wanasiasa kujiepusha na vurugu na wahuni huku taifa hili linapoelekea kwa Uchaguzi Mkuu.

Murkomen alitoa onyo kali kwa waliohusika na shambulizi hilo, akithibitisha kuwa asasi za Sheria tayari zimechukua hatua.

“Ningependa  kuthibitisha kuwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, imewakamata washukiwa watatu, na juhudi zinaendelea kuwatafuta wengine waliona mafichoni,” aliongeza Murkomen.

Waziri huyo aliyasema hayo Leo Ijumaa wakati wa hafla ya mazishi ya Michelle Jelimo Kemboi ambaye ni  bintiye Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Bandari Nchini Nahodha William Ruto.

Aliwataka wanasiasa kushauriana kwa amani, taifa hili linapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu.

Share This Article