Kenya na China zatia saini Mikataba ya Makubaliano

Mikataba hiyo inajumuisha ushirikiano wa kiuchumi, kilimo, ustawi wa mifugo na biashara.

Tom Mathinji
2 Min Read
Kenya na China zatia saini Mikataba ya Makubaliano.

Kenya na China zimetia saini Mikataba ya Makubaliano kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Mikataba hiyo inajumuisha ushirikiano wa kiuchumi, kilimo, ustawi wa mifugo na biashara.

Utiaji saini wa mikataba hiyo ulijiri baada ya mazungumzo kati ya Rais William Ruto na Makamu wa Rais wa China Han Zheng katika Ikulu ya Nairobi.

Kupitia kwa taarifa kwa ukurasa wa X, Rais Ruto alisema Kenya na China zinafurahia uhusiano ulioimarika wa kidiplomasia uliojikita kwa maslahi ya pamoja.

Rais Ruto alidokeza kuwa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kwa maendeleo ya pamoja yatafanikisha bidhaa za Kenya kuingia katika soko la China bila kutozwa ushuru kuanzia mwezi Mei mwaka huu.

Aidha, kiongozi wa taifa aliongeza kuwa ushirikiano uliopo katika kuboresha miundombinu kati ya nchi hizo mbili umeimarisha miradi muhimu ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Narok kuelekea Kisumu na Malaba.

“Ushirikiano wetu katika maendeleo ya miundombinu, unaotekelezwa kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta ya kibinafsi, umefanikisha miradi muhimu kama vile upanuzi wa reli ya kisasa kutoka Narok kuelekea Kisumu hadi Malaba, na barabara kuu ya Rironi-Mau,” alisema Ruto.

Alidokeza kuwa nchi hizo mbili pia zinalenga kuimarisha ushirikiano katika uvumbuzi wa kidijitali, mifumo ya uchukuzi, nishati safi, afya na elimu kwa lengo la kuwanufaisha wananchi.

Share This Article