Kaunti ya Nairobi yashughulukia mafuriko

Hali hiyo ilitokana na mvua kubwa iliyonyesha Nairobi na maeneo mengine nchini.

Marion Bosire
1 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Serikali ya kaunti ya Nairobi imeendelea kuchukua hatua mbali mbali tangu mafuriko kukumba sehemu mbali mbali za jiji la Nairobi Jumamosi alfajiri.

Serikali hiyo ya kaunti ilituma wafanyakazi wake wapatao elfu 4 wa kundi linalofahamika kama “Green Army” ambao wamejukumia kuzibua mitaro ya kupitisha majitaka.

Hatua hii imechukuliwa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Ijumaa usiku na kusababisha mafuriko katika mitaa mbali mbali ya makazi.

Nyumba zilijaa maji, waendeshaji magari wakakwama na wakazi wakafungiwa na mafuriko katika maeneo mbali mbali.

Maeneo ya kaunti ya Nairobi yaliyoathirika ni pamoja na Dagoretti, Parklands, South B, South C, Kariokor, Buruburu, Umoja, sehemu za jiji la Nairobi, Kibra, Nairobi West, Kariobangi South, Eastleigh, Lang’ata na Kamukunji.

Katika taarifa, serikali ya kaunti ya Nairobi ilitangaza pia kutumwa nyanjani kwa makundi 18 ya kushughulikia dharura ya kusaidia katika mipango ya uokoaji na uhamasishaji.

Afisa mkuu wa usimamizi wa majanga Nairobi Bramwel Simiyu amesema kwamba utathmini unaendelea ili kufahamu kiwango kamili cha uharibifu wa mafuriko.

Kulingana na Simiyu, misaada ya kibinadamu itatolewa kwa waathiriwa ikiwemo blanketi na vifaa vingine, punde baada ya tathmini kukamilika.

Share This Article