Mwanasheria mkuu Dorcas Oduor na katibu wa idara ya usalama wa taifa Raymond Omollo wametakiwa kufika mbele ya Mahakama Kuu baada ya uamuzi kugundua kuwa walikiuka amri ya mahakama.
Katika uamuzi wake wa Ijumaa, Jaji John Chigiti alisema kwamba Oduor na Omollo wanalaumiwa kwa kushindwa kutii amri ya mahakama iliyotolewa tarehe 26 Aprili, 2024.
Kesi hiyo inahusisha fidia ya shilingi milioni 1.5 inayodaiwa kwa Robert Ndichu, ambaye alishinda kesi dhidi ya serikali kuhusiana na hukumu iliyotolewa mwaka 2012.
Mahakama ilifahamishwa kwamba licha ya hukumu ya awali, wawili hao hawakujitahidi kuelezea ni kwa nini hawakutii amri ya mahakama wala kuchukua hatua za kutekeleza uamuzi huo.
Hati za mahakama zilibaini kuwa Ndichu alishinda kesi dhidi ya mwanasheria mkuu na serikali mwaka 2009 na alikubaliwa na amri ya mahakama kulipwa shilingi 1,595,605, pesa ambazo hazijalipwa hadi sasa.
Ndichu alidai kuwa licha ya kutumikiwa amri ya mahakama, maafisa hao walipuuzilia mbali wajibu wao wa kisheria.
Jaji Chigiti aliamuru Oduor na Omollo wafike mbele ya mahakama kwa ajili ya upatanishi na hukumu tarehe 23 Juni, 2025.
Hata hivyo, maafisa hao watakuwa na fursa ya kujitetea kabla ya adhabu yoyote kutolewa. Mwaliko huu unajiri wakati ambapo umma umemakinika sana kuhusu viongozi wa umma wanaoshindwa kutii amri za mahakama.