Cardi B atishia kufichua habari mbaya za watu kadhaa akiwemo Offset

Cardi B anasema amechochewa kuafikia uamuzi huo kutokana na hatua ya Offset ya kumchafua kupitia wanablogu

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Cardi B amesema kwamba ana habari mbaya za watu kadhaa akiwemo aliyekuwa mume wake Offset, ambazo anafikiria kufichua.

Cardi B anasema amechochewa kuafikia uamuzi huo kutokana na hatua ya Offset ya kumchafua kupitia wanablogu.

B alikuwa mubashara kwenye mtandao wa X ambapo alimtupia Offset maneno akimwonya kwa kutumia wanablogu kusambaza uvumi kumhusu.

Cardi anasema amekuwa akichokozwa na watu mbali mbali mitandaoni ambao pia wanachokoza watu wa karibu na yeye suala ambalo linamkasirisha sana.

Sasa anasema zamu yake imewadia kwa sababu pepo limemwingia na ni lazima alitoe.

Alimtaja Offset akisema ana marafiki wengi wanablogu ambao wanachapisha habari kumhusu hata ingawa yeye hajawahi kumfanyia hiyo.

Msanii huyo alitaka msamaha kutoka kwa watu kadhaa ambao hakuwataja.

Cardi aliwasilisha ombi la talaka mahakamani Julai 2024, ambapo wakili wake lifafanua kwamba ombi hilo halikutokana na madai ya ukosefu wa uaminifu.

Uhusiano kati ya wawili hao ambao wana watoto watatu umekumbwa na misukosuko ya muda mrefu baada yao kufunga ndoa kisiri mwaka 2017.

Mwaka 2018 ndio walitangazia umma kwamba wameoana na wanatarajia mtoto wao wa kwanza lakini miezi michache baadaye, Cardi B akatangaza kwamba wanatalikiana kwa sababu mapenzi kati yao yalikuwa yamekwisha.

Offset aliamua kuchukua hatua ya kuokoa ndoa yao pale ambapo alimshtukizia Cardi B jukwaano akitumbuiza kwenye tamasha la Rolling Loud akiwa na bango lililokuwa na maandishi ya kumwomba amkubali tena.

Septemba 2020, Cardi B aliwasilisha ombi la kwanza la talaka mahakamani akisema kwamba uhusiano wao ulikuwa umeharibika kiasi cha kutorekebishika.

Inaripotiwa kwamba mama huyo wa watoto watatu sasa alimpata Offset akizini na wanawake wengine lakini akamsamehe na kuondoa ombi la talaka mahakamani.

Mwaka 2023 akiwa mubashara kwenye Instagram, Cardi B alisema kwamba walikuwa wametengana na baba ya watoto wake. Mwaka jana aliwasilisha ombi la talaka mahakamani na siku moja baadaye akatangaza ujio wa mwanao wa tatu.

Website |  + posts
Share This Article