Vifo kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililokumbwa Myanmar na Thailand ni zaidi ya 1,600, kulingana na serikali ya kijeshi ya Myanmar. Haya yanajiri huku waokoaji wakitafuta manusura kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Taarifa rasmi ya serikali hiyo ya kijeshi ilithibitisha vifo 1,644, majeruhi 3,400 na watu 139 hawajulikani waliko baada ya tetemeko hilo la vipimo vya 7.7 vya ritcher.
Mji wa pili kwa ukubwa nchini Myanmar, Mandalay ndo uliathirika zaidi na uko karibu kabisa na kitovu cha tetemeko hilo.
Wakazi wengi wa maeneo yaliyoathirika waliamua kulala nje usiku kwenye kibaridi, wakihofia usalama wao, kufuatia mitetemeko midogo waliyohisi baada ya lile la kwanza.
Barabara zilizoharibika pamoja na majengo yaliyoporomoka vinafanya kazi ya uokoaji kuwa ngumu nchini Myanmar kulingana na afisi ya umoja wa mataifa ya ushirikishi wa masuala ya misaada ya kibinadamu.
Miundomsingi muhimu iliharibiwa kwenye tetemeko hilo kama barabara na madaraja.
Katika taarifa shirika hilo la umoja wa mataifa lilitaja uharibifu wa barabara hasa ile ya kutoka Yangon-Nay Pyi Taw kuelekea Mandalay kuwa kikwazo kikuu katika kazi zao.
Katika hatua inayokusudiwa kushirikisha huduma za uokoaji na usaidizi, serikali ya ziada ya Myanmar inayopinga utawala wa kijeshi imeweka kando tofauti zake na serikali ya kijeshi kwa wiki mbili kuanzia leo Jumapili.
Katika taarifa serikali hiyo ilisema kwamba tawi lake lililojihami la People’s Defence Force (PDF) litashirikiana na umoja wa mataifa na mashirika mengine yasiyo ya serikali kuhakikisha usalama, uchukuzi na kuanzishwa kwa kambi za muda za uokoaji na za huduma za afya.