Marais wa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), wametoa wito wa kukomeshwa kwa vita Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kupitia mkutano kwa njia ya video ulioongozwa kwa pamoja na Rais William Ruto wa Kenya na mwenzake wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, viongozi hao walipokea ripoti ya mkutano wa mawaziri wa EAC na SADC, unaofafanua taratibu za kusitisha vita na uhasama pamoja na kubuni sekretarieti itakayotathmini utekelezwaji wa maamuzi ya mkutano huo wa pamoja.
Wakati wa mkutano huo, Rais Ruto alielezea kujitolea kwa Jumuiya hizo mbili katika kutatua mgogoro huo, ukionya kuwa mzozo huo unasababisha hatari kubwa katika usalama wa kanda hii.
“Hali katika mashariki mwa DRC ni swala la kutiliwa maanani, sio tu kwa DRC kama nchi, lakini kwetu sisi katika Jumuiya ya EAC na SADC, kwa sababu linaweza kuenea katika mataifa jirani,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi kuwa alidokeza kuwa ,“Tunachukua hatua kuhakikisha tunatatua swala hili mashariki mwa DRC<“.
Mkutano huo pia uliwachagua wapatanishi kufanikisha mchakato huo wa amani. Waliochaguliwa ni pamoja na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe, Rais wa zamaniwa Jamhuri ya Afrika ya kati Catherine Samba Panza na aliyekuwa Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inakabiliwa na ukosefu wa usalama katika eneo la Mashariki, yanayosababishwa na makundi ya wapiganaji, wakiwemo wanamgambo wa kundi la M23.