Ni furaha baada ya kina mama zaidi ya 50 waliokuwa wamezuiliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Thika Level 5 kutokana na bili za uzazi kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Gavana Kimani Wamatangi aliwalipia madeni yao, ambayo yalikuwa yamefikia shilingi milioni sita na kuhakikisha kuwa wamerejea kwa familia zao.
Kulingana na afisa wa kamati kuu anayeshughulikia masuala ya afya katika serikali ya kaunti ya Kiambu Elias Maina, baadhi ya kina mama tayari wameidhinishwa kuondoka na wanaendeleza mchakato wa uhakiki.
Wengi wao walisema hawana uwezo kifedha na hawana bima ya afya baada ya mpango wa Linda Mama ambao ulikuwa unafadhili bili za uzazi kusitishwa, huku wengine wakikumbana na matatizo na mpango wa SHA.
Kulingana na uongozi wa hospitali hiyo baadhi ya kina mama ni wageni kutoka nchi kama Burundi na wengine ni watoto wa umri wa chini ya miaka 18 na hivyo hawakuwa na vitambulisho vya uraia.
Dkt. Maina alisema katika muda wa miezi mitatu tu, serikali ya kaunti imeidhinisha msamaha mkubwa, ikiwa ni pamoja na milioni 3 mwezi Agosti 2024 na milioni 4.1 mwezi Septemba 2024.
Aliwasihi watu kujisajili kwa SHA na Kadi ya Wamatangi ili kufaidika na huduma za afya bila malipo.
Josephine Mbeneka, mmoja wa walionufaika, hakuficha furaha yake akisema, “Huduma hapa ni nzuri. Ingawa singeweza kulipa bili”
Rachel Mbogo ambaye mtoto wake alikuwa katika Idara ya NBU, alikuwa na bili ya 196,000 na ameshukuru serikali ya kaunti kwa usaidizi.
Mary Mwende, mkazi wa Juja, pia amesema hivyo, akielezea ukosefu wa uhamasishaji kuhusu mipango ya huduma za afya, ambayo yeye mwenyewe ameahidi kujisajili nayo, akisema kama angekuwa nayo, mzigo usingekuwa mzito hivyo.
Juhudi za serikali ya kaunti ya Kiambu za kuboresha huduma za afya na kujitolea kusaidia wakazi wenye mazingira magumu bado ni imara.
Familia zilizoguswa na hatua hii sasa zina sababu ya kufurahi, kwani wanaanza mwaka mpya wakiwa na matumaini na faraja.