Karen Huger aelezea kutokuwepo katika kikao cha RHOP

Mashabiki wa kipindi hicho walishangaa walipokosa kumwona kwenye kikao hicho wakazua wasiwasi ikabidi ajieleze.

Marion Bosire
2 Min Read
Karen Huger

Karen Huger mmoja wa wahusika wa kipindi cha ‘The Real Housewives of Potomac’ ameelezea sababu yake ya kutokuwepo kwenye kikao msimu wa tisa wa kipindi hicho.

Katika taarifa, meneja wake aitwaye Ryan Tresdale alielezea kwamba Karen aliamua kuingia kwenye kituo cha kibinafsi cha urekebishaji tabia.

“Tunasimama na Karen wakati huu ambao anaanza safari ya maana ya kupona na tunafurahia aliafikia uamuzi huu.” aliendelea kusema Tresdale.

Hatua hii inafuatia tukio la Karen kupatikana na hatia kwenye makosa kadhaa baada yake kushtakiwa kwa kuendesha gari akiwa mlevi mwezi Machi mwaka jana huko Maryland.

Wakili wa Karen kwa jina A. Scott Bolden, naye alitoa taarifa Disemba 18, 2024, baada ya jopo la waamuzi kuafikia uamuzi katika kesi hiyo.

“Hata ingawa hatujaridhika na uamuzi huu, tunauheshimu na kushukuru kwa kutumia muda wao kusikiliza kesi yetu.” alisema Bolden.

Wakati huo aliashiria kwamba walikuwa na mipango ya kukata rufaa kuhusu uamuzi huo akisema ni haki ya Karen huku akishukuru mashabiki zake kwa kuendelea kumwombea.

Karen alishtakiwa kwa kuendesha gari akiwa mlevi na makosa mengine kama kuendesha gari vibaya, kuendesha gari kwa kasi, kuendesha gari akitumia leseni ambayo ilikuwa imesimamishwa na kukosa kufahamisha maafisa kuhusu kubadilisha makao.

Alipatikana na hatia kwenye makosa yote isipokuwa kuendesha gari vibaya kwenye kesi hiyo iliyosikilizwa na kuamuliwa kwa siku mbili tu, kuanzia Disemba 17, 2024.

Kikao cha kumhukumu kinatarajiwa kuandaliwa Januari 29, 2025.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *