Mahakama Kuu ya Eldoret imemhukumu afisa wa zamani wa polisi miaka 30 gerezani, baada ya kumpata na hatia ya kumuua mke wake.
Bernard Ndege ambaye alikuwa na cheo cha konstabo, anadaiwa kumpiga risasi mke wake mara 11 akitumia bunduki aina ya AK47, na kumuua papo hapo.
Jaji wa mahakama hiyo Reuben Nyakundi, alimpata Ndege na kosa hilo, baada ya mashahidi sita kuwasilisha ushahidi wao mahakamani.
Tukio hilo la mauaji ya Fenny Bosibori, lilitekelezwa Machi 9, 2019 katika makazi ya maafisa wa polisi kwenye kituo cha polisi cha Soy, kaunti ya Uasin Gishu..
Afisa aliyekuwa akichunguza kesi hiyo, alithibitisha kuwa Ndege alikuwa amepewa risasi 30, lakini ni risasi 19 pekee zilizopatikana katika eneo la mkasa.
Akimhukumu Ndege, Jaji Nyakundi alisisitiza uzito wa kesi hiyo, akidokeza jukumu ambalo afisa huyo alipaswa kutekeleza la kudumisha sheria.