Rais William Ruto amewaongoza viongozi wengine nchini kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR Roseline Odede.
Kwenye taarifa, Ruto amemtaja Odede kama mtu aliyekuwa shupavu katika kupigania haki za binadamu.
“Nimehuzunishwa mno na kifo cha mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR Roseline Odhiambo Odede,” alisema Ruto.
“Odede alikuwa shujaa shupavu wa kupigania jamii yenye usawa na haki.”
Chama cha Wanasheria nchini, LSK pia kimemlimbikizia sifa marehemu Odede kikimtaja kuwa mtu aliyechapa kazi yake kwa uadilifu.
“Uongozi wa Roseline kwenye KNCHR ulikuwa wenye ujasiri na dhamira ya kupigania utawala wa sheria na haki za binadamu,” alisema Faith Odhiambo, mwenyekiti wa LSK kwenye taarifa.
“Aliiongoza tume hiyo wakati wa kipindi kigumu cha haki za binadamu nchini Kenya lakini akasimama kidete dhidi ya uvunjaji sheria bila kujali na utawala mbaya. Kifo chake ni pigo kubwa kwa nchi na jumuiya ya watetezi wa haki za binadamu.”
Matamshi sawia yaliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga.
“Odede alikuwa mtu mwenye heshima na mwenye msimamo thabiti katika utekelezaji wa majukumu yake,” alisema Ingonga kwenye salamu zake za rambirambi.
Wengine waliomlimbikizia sifa Odede kama mtu aliyekuwa shupavu katika utendakazi wake ni Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo.
Odede alifariki jana Ijumaa baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kifo chake kilitangazwa leo Jumamosi na Naibu wake Raymond Nyeris.
Nyeris ametaja kifo hicho kuwa pigo kubwa kwa tume hiyo.
Mrehemu Odede alikuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya na pia awali alihudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Kuwapiga Msasa Majaji na Mahakimu.
Alikuwa wakili kwa zaidi ya miaka 30.