Ndindi Nyoro atimuliwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti

Martin Mwanje
1 Min Read
Ndindi Nyoro - Mbunge wa Kiharu

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ameondolewa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Taifa. 

Mahali pake pamechukuliwa na mbunge wa Alego Usonga Sam Atandi.

Mbunge wa Endebess Robert Pukose amechaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Jana Jumanne, kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah aliwaongoza wabunge katika kumshambulia Nyoro, akiwasihi wabunge kumtimua kwenye wadhifa huo

Katika kutoa wito huo, Ichung’wah alidai Nyoro alijilimbikizia fedha nyingi alizotumia kustawisha eneo bunge lake wakati akiyatelekeza maeneo mengine nchini.

Nyoro hajajibu madai hayo hadi kufikia sasa.

Masaibu ya mbunge huyo wa Kiharu yalianza wakati wa kufurushwa kwa Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.

Wakati wabunge wa muungano tawala wa Kenya Kwanza wakiunga mkono waziwazi kutimuliwa kwa Gachagua, Nyoro alidumisha kimya kingi mno.

Hatua hiyo ilichukuliwa kumaanisha aliegemea mrengo wa Gachagua.

Wabunge waliomuunga mkono Naibu Rais huyo wa zamani wakati wa mchakato wa kumwondoa madarakani wamefurushwa katika uongozi wa kamati mbalimbali za bunge.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *