Kesi ya Keefe D yaahirishwa tena

Keefe D anahusishwa na mauaji ya mwanamuziki Tupac Shakur.

Marion Bosire
2 Min Read
Keefe D

Mashabiki wa marehemu Tupac Shakur watalazimika kusubiri kwa muda zaidi hadi kesi ya jamaa anyeshukiwa kutekeleza mauaji yake ianza.

Haya yanajiri baada ya mawakili wa jamaa huyo kwa jina Keefe D, kuwasilisha ombi mahakamani la kutaka muda zaidi wa kuchunguza kesi ya mteja wao.

Kesi dhidi ya Keefe D ilikuwa imepangiwa kuanza kusikilizwa katikati ya mwezi Machi mwaka huu wa 2025 lakini sasa imesongeshwa hadi Februari 2026.

Jaji alitoa uamuzi huo katika kikao kilichoandaliwa Jumanne.

Katika kikao hicho, jaji Carli Kierny alisema kwamba inaonekana kuna mambo kadhaa ambayo hayajafanywa katika kuandaa kesi hiyo ili Keefe Davis apate usaidizi wa wakili.

Jaji Kierny alisema hakuwa na chaguo jingine ila kuwapa muda watetezi wa mshukiwa.

Wakili wa Keefe D, Carl Arnold, alisema sababu kuu ya kuomba muda zaidi ni kupata fursa ya kudadisi mashahidi wapya ambao huenda wakathibitisha kwamba Keefe wa miaka 61, hakuwa katika eneo la mauaji ya Shakur Septemba 7, 1996.

Duane Davis almaarufu “Keffe D” alikamatwa kuhusiana na mauaji ya Shakur Septemba 29, 2023, waendesha mashtaka wakiamini kwamba aliamuru mauaji hayo.

Alikanusha mashtaka dhidi yake mbele ya mahakama mnamo Novemba 2, 2023 na kesi ikapangiwa kuanza Juni 3, 2024, lakini ikaahirishwa hadi Novemba 4, 2024.

Mahakama ilimpa mshukiwa huyo dhamana ya dola elfu 750 na kifungo cha nyumbani Januari 9, 2024 lakini mpaka sasa amezuiliwa katika jela ya jimbo la Clark.

Mwaka 2018, Davis alikubali hadharani kwamba alikuwa kwenye gari ambalo lilikuwa limebeba aliyefyatua risasi zilizomuua Tupac Shakur.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *