Hashim Dagane ahusishwa na kisa kingine cha mauaji

Tom Mathinji
1 Min Read
Hashim Dagane ahusishwa na kisa kingine cha mauaji.

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wamemhusisha mshukiwa wa mauaji ya watu watatu eneo la Eastleigh Hashim Dagane,na kisa kingine cha mauaji.

Maafisa hao wamemhusisha Dagane na mwili uliopatikana umetupwa katika makaburi ya Lang’ata Oktoba 31,2024.

Walipokuwa wakitekeleza uchunguzi wao, maafisa hao walielekea katika duka la jumla la Quickmart ambako mwathiriwa huyo anadhaniwa kuwa mwanamke alinakiliwa na kamera fiche za CCTV akinunua bidhaa Oktoba 29,2024.

Baadaye, ilibainika kuwa baada ya kununua bidhaa, mwathiriwa huyo aliingia katika jengo mtaani Lavington, ambako pia alinakiliwa na kamera za CCTV.

Baada ya uchunguzi wa kina, ilibainika kuwa mwanamke huyo alikuwa ameandamana na Hashim Dagane, ambaye anaishi katika jengo hilo.

Siku iliyofuatia Oktoba 31,2024, Dagane alinakiliwa na kamera hizo akitoka katika jengo hilo akiwa amebeba mifuko miwili inayoaminika kuwa mwili wa mwanamke huyo.

Mifuko hiyp ilipatikana baadaye siku hiyo hiyo katika makaburi ya Lang’ata.

Kulingana na maafisa hao wa DCI, baada ya mwenye jengo hilo kugundua kilichofanyika, alisafisha nyumba alimolala Dagane na mwathiriwa huyo wa kike na kulipaka rangi upya na kutoweka.

Mwenye jengo hilo pia anasakwa na maafisa wa polisi, ili afunguliwe mashtaka.

Mwathiriwa huyo wa kike anaaminika kuwa Deka Abdinoor Gorone, aliyeripotiwa kutoweka Oktoba 24,2024.

TAGGED:
Share This Article