Rais William Ruto, amewasili Jijini Juba, Sudan Kusini, kushiriki mazungumzo na mwenyeji wake Rais Salva Kiir Mayardit, kuhusu mchakato wa amani almaarufu Tumaini.
Mkutano huo unajiri, baada ya Rais wa Sudan Kusini kuzuru taifa hili Agosti 27, 2024, alipohudhuria mkutano wa kumzindua mwaniaji wa Kenya kwenye wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika AUC.
Juma lililopita, Rais Ruto alijadiliana na ujumbe kutoka Sudan Kusini na pia alikutana na wawakilishi wa upande wa upinzani wa taifa hilo, kupitia mchakato wa amani wa Tumaini Jijini Nairobi.
Kulingana na katibu wa mawasiliano wa Rais Emmanuel Talam,marais hao wawili watajadili mafanaikio yaliopatikana chini ya mpango wa amani wa Tumaini.
Mpango huo wa upatanishi ulioasisiwa jijini Nairobi mwezi Mei mwaka huu, unawashirikisha viongozi mbali mbali.
Marais Ruto, Kiir na aliyekuwa komanda wa jeshi la nchi kavu la Kenya Meja jenerali Lazarus Sumbeiywo, ndio wapatanishi wakuu.
Mpango huo wa amani pia unajumuisha makundi mengine ambayo hayakusaini mkataba wa amani wa mwaka 2018.