Rais William Ruto kwa sasa anaongoza sherehe za mwaka huu za Siku ya Mashujaa zinazoandaliwa katika Uwanja wa Kwale, katika kaunti ya Kwale.
Hii ni mara ya kwanza kwa sherehe hizo kuandaliwa katika kaunti hiyo.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya sherehe hizo ni “Boma Langu, Nyumba Yangu, Mimi ni Shujaa.”
Punde baada ya kuwasili, Rais aliitikia salamu kutoka kwa raia wanaohudhuria sherehe hizo kabla ya kukagua gwaride la heshima.
Viongozi mbalimbali wakiwemo Mama wa Taifa Rachel Ruto na Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki wanahudhuria sherehe hizo.
Wengine wanaozihudhuria ni Magavana kutoka eneo la Pwani, Mawaziri, Wabunge, Makatibu na Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali humu nchini.