Askofu Benson Gathungu Kamau maarufu kama Muthee Kiengei leo amefanya mkutano na mwanamitandao Pritty Vishy na usimamizi wake baada ya kukashifiwa vikali mitandaoni kwa matamshi dhidi yake.
Video ilisambaa mitandaoni ikimwonyesha Kiengei akihojiwa huku akizungumzia maumbile ya Vishy akimtaja kuwa mnene na hivyo hana mvuto.
Vishy alitumia mitandao hiyo hiyo kuzungumzia suala hilo ambapo alisema kwamba Jumapili angefika kwenye kanisa la JCM linalosimamiwa na Kiengei ili amwambie maneno aliyasema kwenye video uso kwa uso.
Wanamitandao wengine wengi walighadhabishwa pia na usemi wa JCM wakisema hastahili kuwa muhubiri iwapo anaweza kufanyia mzaha maumbile ya mtu huku akicheka.
Mwanamke ambaye alikuwa akimhoji Kiengei kwa jina Lizz Wangui kwenye runinga ya kanisa la JCM naye hakusaazwa mitandaoni kwani wengi wanashangaa ni kwa nini alikuwa akicheka huku mwanamke mwenzake akidhalilishwa kwa sababu ya maumbile yake.
Wafuasi wengi wa Vishy walijitolea kwenda naye Jumapili kwenye kanisa la JCM kuwajibisha askofu huyo.
Kiengei alilazimika kuomba msamaha kutokana na matamshi yake na leo amefanya mkutano na Vishy na usimamizi wake ingawa bado taarifa kuhusu waliyoafikiana bado hazijawekwa wazi.
Picha zilizochapishwa mitandaoni zinaonyesha Vishy, Kiengei na watu wengine wengi wakila kwenye kile kinachoonekana kama hoteli.