Mamlaka ya kitaifa ya kampeni dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya NACADA), imetangaza kuanzisha msako kote nchini unaolenga kufunga baa na maeneo ya kuuza pombe yaliyo karibu na taasisi za elimu.
Kupitia kwa ujumbe wake siku ya Jumatatu, NACADA imesema msako huo umejikita katika Sheria ya Kudhibiti Ulevi ya mwaka 2010, ambayo inaeleza kuwa baa zinapaswa kuwa umbali wa zaidi ya mita mia tatu, kutoka kwa shule za chekechea, msingi na upili au taasisi nyingine za elimu zinazohudumia watu wa chini ya umri wa miaka kumi na minane.
“NACADA inatangaza msako kote nchini unaolenga kutekeleza kanuni kuhusu biashara za baa na vituo vingine vya kuuza pombe karibu na taasisi za elimu au maeneo yanayohudumia watu walio chini ya umri wa miaka kumi na minane,” ilisema taarifa ya NACADA .
Msako huo utatekelezwa kwa ushirikiano na wakala husika wa Serikali ya Kitaifa na Kaunti na unalenga kuhakikisha utiifu mkali wa matakwa ya kisheria kuhusu baa na maduka ya kusambaza vileo.
Mamlaka hiyo imetoa onyo kali kwa wale watakaokiuka agizo hilo.
“Sheria ya Kudhibiti vileo ya mwaka 2010 pia inatoa maelezo kuhusu adhabu kwa mtu yeyote anayeuza vileo katika maeneo yaliyopigwa marufuku kuwa watatozwa faini isiyozidi shilingi laki tano, au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja,” ilionya NACADA.
Agizo hilo limetolewa wiki moja baada ya mamlaka hiyo kuamuru kuondolewa kwa mabango ya matangazo ya vileo karibu na taasisi za masomo.