Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kisii Dorice Aburi, ametoa wito kwa washikadau mbalimbali kusaidia watu walio na ulemavu kupitia programu za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika shule maalum ya Kerina katika kaunti ndogo ya Kisii Kaskazini, Aburi aliwahimiza wazazi kuwasajili watoto wao wenye ulemavu, ili wanufaike na mipango ya watu wenye ulemavu inayofadhiliwa na ofisi yake.
“Ofisi yangu ipo wazi kwa kila mtu. Wazazi wachangamkie fursa hii ili tuweze kutatua changamoto zinazowakumba watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kutoa misaada ili kuwarahisishia fursa ya kupata elimu,” alisema.
Hafla hiyo iliyopewa jina la ‘ Donya Charity Mission’, ilijumuisha kutolewa kwa mchango wa shilingi 200,000 na usambazaji wa zaidi ya baiskeli 80 na viti vya magurudumu kwa familia zilizo na uhitaji kupitia usaidizi wa heri.
Aburi aliwataka viongozi wa eneo hilo kuwa mstari wa mbele katika kutoa programu zinazowainua watu wenye ulemavu.
Aidha aliwataka wakumbatie ushirikishwaji wa umma, ili kuelewa na kushughulikia baadhi ya changamoto zinazowakabili wakazi wa kaunti ya Kisii, zikiwemo miundombinu duni ya barabara, ukosefu wa umeme na uhaba wa maji.
Akizungumza katika hafla hiyo, mfanyabiashara Kevin Aruasa alimpongeza mwakilishi huyo wanawake kwa mpango huo na kuahidi kuwakusanya wafanyabiashara na wanawake wengine kusaidia watu wanaoishi na ulemavu.
“Kama una mtu anayeishi na ulemavu hii ni nafasi yako ya kuwatoa nje ili waweze kusaidiwa, tuache unyanyapaa,” alisema.