Kocha wa Harambee Stars Engin Firat amemtema nahodha Michael Olunga kwenye kikosi cha wachezaji 25 kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Burundi na Ivory Coast mwezi ujao.
Kocha Firat amewajumuisha wachezaji wengi walioshiriki mashindano ya mataifa manne nchini Malawi, mwezi Machi mwaka huu.
Wachezaji wapya walioshirikishwa kikosini kwa mara ya kwanza ni mlinzi wa Kenya Police Brian Okoth na Adam Wilson, anayecheza soka ya kulipwa na klabu ya Bradford City nchini Uingereza.
Wengine waliopata nafasi hiyo ni kiungo wa Gor Mahia Austine Odhiambo, Tobias Knost anayechezea SV Verl nchini Ujerumani na Bruce Kamau anayechezea timu ya Perth Glory nchini Australia.
Waliorejeshwa kwenye kikosi baada ya kukosa safari ya Malawi mwezi Machi ni Elvis Rupia na Duke Abuya.
Stars itacheza mechi hizo za kufuzu Kombe la Dunia 2026 na Burundi Juni 7, 2024 kabla ya kuwaalika Ivory Coast Juni 11, 2024.
Kikosi cha Firat kinatarajiwa kuanza mazoezi ya kujiandaa Jumanne Mei 21 jijini Nairobi, kabla ya kusafiri kwenda jijini Lilongwe, Malawi ambapo watacheza mechi hizo uwanjani Bingu .
Mechi za nyumbani za Kenya zimepelekwa Malawi kwa kuwa viwanja vya Nyayo na Kasarani, ambavyo vimeidhinishwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuandaa mechi za kimataifa, vimefungwa kwa ukarabati.
Viwanja hivyo vitaandaa michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kikosi hicho cha muda.
Makipa
Patrick Matasi (Kenya Police), Byrne Odhiambo (Bandari), Boniphas Munyasa (Muranga Seal), Ian Otieno (Zesco, Zambia)
Walinzi
Johnstone Omurwa (Estrela, Portugal), Alphonse Omija (Dhofar-Oman), Amos Nondi (Ararat, Armenia), Brian Okoth (Kenya Police), Abud Omar (Kenya Police), Tobias Knost (SV Verl, Germany)
Viungo
John Ochieng (Zanaco, Zambia), Eric Johanna (UTA, Romania), Adam Wilson (Bradford City, England), Anthony Akumu (Unattached), Kenneth Muguna (Kenya Police), Kaycie Odhiambo (AFC Leopards), Chrispine Erambo (Tusker), Rooney Onyango (Gor Mahia), Ayub Timbe (Sabail, Azeberijan), Duke Abuya (IHEFU, Tanzania), Bruce Kamau (Perth Glory, Australia)
Washambulizi
John Avire (El Sekka El Hadid SC, Egypt), Austine Odhiambo (Gor Mahia), Benson Omala (Gor Mahia), Elvis Rupia (IHEFU, Tanzania)