Wakazi wa Garissa wanakumbwa na upungufu wa bidhaa muhimu kufuatia kufungwa kwa barabara kuu ya Garissa – Madogo kutokana na mafuriko.
Tangu siku ya Ijumaa jioni, shughuli za uchukuzi zimekatizwa, ikiwa vigumu kwa watu na mizigo kuingia au kutoka mji wa Garissa.
Huku barabara hiyo ikiwa kiingilio katika eneo la Kaskazini Mashariki, wasafiri wanaoelekea Wajir na Mandera pia wamekwama katika mji wa Magodo.
Hii ni mara ya tatu kwa barabara hiyo kutatiza shughuli za uchukuzi, baada ya kuharibiwa na mvua ya El Nino mwezi Disemba mwaka 2023.
Maeneo yaliyoathirika pakubwa ni pamoja na daraja la mto Tana, Mororo na Kona Punda, ambapo njia mbadala za muda zimetenegenezwa.
Halmashauri ya ujenzi wa barabara kuu hapa nchini kupitia ukrasa wake wa X, imetangaza kufungwa kwa barabara hiyo, huku ikiwaonya wananchi kusubiri maji yapungue kabla ya kuvuka eneo hilo.
“KeNHA inawafahamisha umma kuwa barabara kati ya Garissa na Madogo imefungwa kwa watumiaji wote hadi viwango vya maji vitakapopungua na ukarabati wa sehemu iliyoharibika utakapokamilika,” ilisema taarifa ya KeNHA.