Dorcas Rigathi aomboleza na familia zilizowapoteza wapendwa wao Kirinyaga

Tom Mathinji
1 Min Read
Mke wa naibu Rais Dorcas Rigathi awataka wanawake kufunga baa zote kaunti ya Kirinyaga.

Mkewe naibu Rais mchungaji Dorcas Rigathi, ametoa wito kwa wanawake na makanisa kushirikiana katika harakati za kupambana na unywaji wa pombe haramu ambayo imesababisha vifo vya watu 13 na kuwaacha wengine wakiwa wamepoteza uwezo wa kuona katika kaunti ya Kirinyaga.

Akizungumza katika kijiji Kangai  siku ya Jumamosi baada ya kutembelea familia zilizopoteza wapendwa wao waliofariki baada ya kubugian pombe hiyo, Dorcas aliwataka wanawake kuunga serikali mkono kukabiliana vilivyo na pombe haramu.

“Unaenda kwenye baa, unanunua kifo, na pia unanunua machozi kwa familia nzima. Mimi nikiwa mchungaji, nimechoka kuwazika watoto na waume kutokana na vifo vinavyosababishwa na pombe,” alisema mchungaji Dorcas.

Aidha mchungaji Dorcas ambaye ni mojawapo ya wanaharakati walio katika mstari wa mbele kupinga utengenezaji, usambazaji na unywaji wa pombe pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, alitoa wito kwa makanisa kutoa nafasi za kazi kwa vijana ili kuwaepusha na unywaji wa pombe na matumizi ya dawa za kulevya.

Alitoa wito kwa wanawake kufunga baa zote zilizosalia ili kulinda kizazi kilichosalia.

Viongozi mbalimbali wa kanisa ambao wanajumuisha wainjilisti, wachungaji na maaskofu waliombea familia hizo, jamii na taifa lote kwa ujumla ili Mungu awakinge dhidi ya matumizi ya pombe, dawa za kulevya na   biashara za kuuza pombe haramu.

Share This Article