Jaji Fatuma Sichale ameapishwa kuwa mwanachama wa Tume ya Huduma za Majaji, JSC.
Atakuwa mwakilishi wa Mahakama ya Rufaa kwenye tume hiyo na anajaza pengo lililoachwa na Jaji Mohammed Warsame anayeoondoka baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka 10.
Jaji Sichale alikula kiapo cha uanachama wa JSC wakati wa halfa ya uapishaji iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome leo Jumatatu asubuhi.
“Leo unajiunga na makamishna wengine wa JSC katika wajibu wetu wa pamoja wa kuhakikisha uhuru na uwajibikaji wa idara ya mahakama kama ilivyoelezwa katika Kifungu 172 cha Katiba,” alisema Jaji Koome wakati wa hafla hiyo.
“Majukumu yote ya JSC hatimaye yanakuwa kitu kimoja ambacho ni kuwezesha kufikiwa kwa haki ya “kupata haki” kama ilivyoelezwa katika Kifungu Namba 48 cha Katiba, ambayo ndio lengo kuu la idara ya mahakama. Nina uhakika utafanya kazi vyema na wenzako katika Tume katika kuhakikisha utimizaji wa mamlaka ya kikatiba ya JSC.”
Jaji Koome alimsifia Jaji Warsame kwa kuwa mchapa kazi kwa kipindi cha miaka 10 alichohudumu, akitaja mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika JSC na idara ya mahakama kwa jumla.