Majina ya kiingereza ya Raila na Oburu Oginga yafichuliwa

Marion Bosire
2 Min Read

Majina ya viongozi wawili wa familia ya marehemu Jaramogi Oginga Oding, Raila Odinga na Oburu Oginga yamefichuliwa.

Haya yalifanyika jana Jumamosi, Januari 20, 2024 kwenye hafla ya kumkumbuka Mzee Jaramogi katika ukumbi wa Ofafa mjini Kisumu, miaka 30 tangu alipofariki.

Dada ya Raila na Oburu kwa jina Wenwa Akinyi ndiye alifichua majina hayo akisema kwamba baada ya ubatizo, Raila alipatiwa jina “Joshua” na Oburu akapatiwa jina la “Caleb” huku Mzee Jaramogi akipatiwa jina la “Nicodemus”.

Kabla ya hapo, Akinyi alielezea kwamba yeye na wenzake walijaribu kujipa majina ya Kiingereza ambapo yeye alijichagulia jina “Jennifer” lakini tena akaliacha.

Wakati wa kujiunga na shule ya upili, Akinyi alijipa jina jingine la Roselyn lakini baadaye aliamua kuliacha na kuchukua majina aliyompa babake.

Oburu alikuwa amejipa jina “John Dennis” na Beryl akajibandika “Jane Alice” lakini wote walikuwa wanaogopa kujuza wazazi majina hayo.

Mzee Jaramogi hakuwa anapendelea majina ya Kiingereza.

Wenwa Akinyi alifafanua kwamba Jaramogi hakuchukia wazungu ndiposa akaamua kutumia majina ya kiasili pekee bali alitaka tu kuendeleza utamaduni.

Anaandika kitabu kuhusu familia yao na anasema mambo mengi yameelezewa kwa kina humo kwa hivyo watu wajiandae.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wengi akiwemo Waziri Moses Kuria, Gavana wa Kisumu Profesa Anyang Nyong’o na mkewe, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir, Daktari Mukhisa Kituyi, aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Ambetsa Oparanya, viongozi wa upinzani bungeni na wengine wengi.

 

 

Share This Article