ODM yataka Kamanda wa polisi kaunti ya Kisii ahamishwe

Tom Mathinji
1 Min Read

Chama cha ODM sasa kinataka kuhamishwa mara moja kwa kamanda wa polisi wa kaunti ya Kisii, Charles Kesses, kufuatia kile chama hicho kimedai kuwa majaribio ya kumuua gavana wa kaunti hiyo Simba Arati.

Akiwahutubia wanahabari katika afisi za idara ya maafisa wa upelelezi wa jinai DCI kaunti ya Kisii, katibu mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna, alitoa makataa ya siku 14 kwa serikali kuangazia suala hilo, la sivyo chama hicho kitachukua hatua.

Kadhalika katibu huyo ametoa wito wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa maafisa wa polisi waliozua rabsha wakati wa hafla ya kutoa ufadhili wa masomo iliyoongozwa na gavana Arati.

Aidha Sifuna amewataka polisi kuchunguza mwanasiasa mmoja wa eneo hilo na baadhi ya maafisa wa polisi kwa kuchochea ghasia, huku akiitaka halmashauri huru ya usimamizi wa huduma ya taifa ya polisi, IPOA kuchunguza utumiaji mbaya ya maafisa wa polisi katika kaunti ya Kisii.

Shirika la utangazaji la KBC lilimtafuta Kamanda wa polisi wa eneo la Nyanza Manasse Musyoka, lakini hakutoa kauli yoyote kuhusu suala hilo.

Share This Article