Waziri wa mawasiliano na uchumi dijitali Eliud Owalo na mwenzake wa biashara Rebecca Miano kesho watanzindua mkakati wa mwaka 2023 wa biashara ya mtandaoni almaarufu “E-commerce”.
Mkakati huo unalenga kuendeleza uchumi dijitali na unalenga kubadilisha mfumo wa biashara ya mtandaoni kupitia kukuza uvumbuzi ujumuishaji na hatimaye ukuaji wa uchumi.
Kulingana na taarifa ya Mulei Muia ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano ya umma, mkakati huo uliafikiwa kwa ushirikiano kati ya serikali, sekta ya kibinafsi na wataalamu wa sekta hiyo kwa lengo la kuafikia ufanisi kamili wa uchumi dijitali nchini Kenya.
Muia anaelezea kwamba unawiana na ajenda ya serikali ya kukuza uchumi wa watu wa tabaka la chini kuelekea tabaka la juu almaarufu “Bottom-Up Economic Transformation Agenda – BETA”.
Kando na hayo mkakati huo unaangazia haja ya Kenya kuwa kitovu cha biashara ya mtandaoni katika kanda na kuwezesha biashara ya kuuza nje ya nchi na kununua kutoka nchi nyingine na kuishia kutoa fursa za ajira, kuwa kitega uchumi na kupunguza umaskini.
Utaboresha pia upatikanaji wa bidhaa na huduma za Kenya katika masoko ya ulimwengu hasa zile za miashara ndogo na za kadri.
Hafla ya kuzindua mkakati huo wa kitaifa kuhusu biashara ya mtandaoni itaandaliwa kesho jioni ambapo wahusika wakuu wa sekta hiyo watakongamana.
Kutakuwepo na hotuba na hata kipindi cha mtagusano kwa lengo la kukuza majadiliano na ushirikiano kati ya wahusika ili kuhakikisha utekelezaji mwafaka wa mkakati huo.