Serikali imetakiwa kuharakisha mpango wa marekebisho ya kanuni za ushirikiano baina ya sekta za umma na za kibinafsi ili kuanza upanzi wa mchele kwa kiwango kikubwa katika mradi wa unyunyiziaji mashamba maji wa Tana Delta.
Mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Ustawishaji wa Miradi ya Mito ya Tana na Athi (TARDA) una uwezo wa kulima zaidi ya ekari 30,000 ya mchele.
Mradi huo uliathirika pakubwa na janga la mafuriko lakini kwa sasa, marekebisho yako karibu kukamilika na kuwezesha shughuli za ukuzaji mchele kuanza tena.
Kamati ya Halmashauri ya Maendeleo ya Mikoa imezuru mradi huo huko Tana Delta na ikaomba serikali kuharakisha kutafuta wawekezaji wa kibinafsi ili waanze kupanda mchele kwa wingi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Peter Lochakapong amesema serikali inafaa kuharakisha mpango huo ili waweze kunufaika na mazao ya mradi huo.
Aidha amepinga mpango wa kufutilia mbali Halmashauri za Maendeleo ya Mikoa na kuomba kamati husika kuchukua maoni kwa wingi kutoka kwa wananchi katika maeneo husika ili waweze kupata mwelekeo thabiti.