Watu 10 wameshtakiwa kwa kosa la udanganyifu wa uuzaji ardhi wa shilingi bilioni moja jijini Nairobi.
Kisa hicho kimekuwa kikichunguzwa kwa muda na Kitengo cha Upelelezi wa Ulaghai wa Ardhi cha Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI.
Miongoni mwa washukiwa hao kumi ni Jacob Cartwright Owino ambaye ni Msajili wa Hatimiliki katika makao makuu ya Wizara ya Ardhi yaliyopo katika jumba la Ardhi jijini Nairobi na Andrew Aseri Kirungu ambaye ni afisa wa usimamizi wa ardhi. Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka zaidi ya kutumia vibaya mamlaka yao.
Kulingana na DCI, mpango uliotibuka wa kuuza ardhi hiyo ulihusisha wawili hao pamoja na watu wengine ambao ni Diana Njeri Muiyuro, James Mbote Gicheha, Joseph Njoroge Kimani na Joseph Gichohi Kinyanjui.
Wengine ni Gladys Wambui Mwangi, Mohamed Jimale Abdille, Charles Mwangi Waithaka na George Ndungu Mumbi.
Wote hao wanasemekana kupanga njama ya kulaghai kampuni ya Realty Brokers Limited kipande cha ardhi cha mamilioni ya pesa kwa kusingizia kuwa barua ya ugavi wa ardhi hiyo Ref. No. 93103 ilikuwa ya kweli na kwamba ilitolewa na Tume ya Kitaifa ya Ardhi kwa lengo la kuwezesha kusajiliwa kwa ardhi hiyo katika jina la Mwadi Women Entrepreneurs Limited.
Mashtaka mengine wanayokabiliwa nayo washukiwa hao 10 ni kutengeneza nyaraka ghushi na kupata usajili kupitia udanganyifu.
9 kati ya washukiwa hao walikanusha mashtaka walipofika mbele ya Hakimu Mkuu Lucas Onyina na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 100,000 pesa taslimu. Kirungu hakufika mahakamani kwa msingi kwamba aliugua.