Mwanamuziki wa Tanzania Zuhura Othman Said almaarufu Zuchu amemshauri mamake mzazi ambaye pia ni mwanamuziki Khadija Kopa apoze moyo wake.
Ushauri wake unafuatia mawasiliano ya simu kati ya Khadija na mdaku wa mitandaoni nchini Tanzania MaiMartha, ambapo Kopa alisikika akimwonya akome kumsema mwanawe.
Kopa alighadhabishwa na usemi wa MaiMartha kwamba Zuchu hana heshima na watu wa familia ya mpenzi wake Diamond Platnumz.
Akizungumza na wanahabari huko Zanzibar ambapo amekita kambi kwa ajili ya tuzo za Trace, Zuchu alisema kwamba hakufahamu kilichokuwa kikiendelea mitandaoni.
“Unajua mimi sikuwa najua chochote! Unajua mimi ndio wa mwisho kufahamu. Timu yangu inanijua kwa hivyo huwa hawaniambii kitu. Nitakwambia hili, nimesikia hiyo sauti ikabidi nimpigie mama simu.” alisema Zuchu.
Aliendelea kuelezea kwamba alimpigia simu mamake kufahamu kilichokuwa kimemkasirisha na anasema huo ni ukuaji tu wa kurasa na majukwaa ya umbea mitandaoni.
“Kwa sababu tunakaa tofauti anaweza akahisi mwanangu huko aliko anaandamwa nitampiga kila mtu. Kumbe maskini niko zangu nyumbani nakula vizuri nacheka.” aliendelea kusema Zuchu.
Mwanamuziki huyo sasa anamtaka mamake apoze moyo akisema, “Pole ndio hivyo umezaa mtoto maarufu, ndizo changamoto zinazokuja na watu wako kwenye kazi zao wanataka kukuza majukwaa yao ili maisha yao yaende.”
Nyota huyo alimalizia kusema kwamba sio kila kitu mitandaoni ni cha kweli akihimiza watu waache wambea wa mitandao waendelee kukuza majukwaa yao.