Zaidi ya watu 50 wanahofiwa kuaga dunia, baada ya lori kugonga magari kadhaa katika makutano ya Londiani, katika barabara ya Kericho-Nakuru.
Wanabiashara waliokuwa kando ya barabara hiyo pamoja na wahudumu wa Boda Boda, ni miongoni mwa waathiriwa wa ajali hiyo, iliyotokea Ijumaa jioni.
Naibu Gavana wa Kericho Fred Kirui, alisema wamewatuma wahudumu wa afya pamoja na magari ya kuwabeba wagonjwa kusaidia katika shughuli ya uokoaji.
Mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha katika eneo hilo, ilitatiza shughuli za uokoaji, huku ajali hiyo ikisababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara hiyo.
Afisa mkuu wa polisi wa Londini Agnes Kunga, alisema idadi kamili ya walioangamia katika ajali hiyo itathibitishwa baada ya kukamilika kwa shughuli za uokoaji.
Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen, alituma risala za rambi rambi kwa familia ya walioangamia katika ajali hiyo.
“Nachukua fursa hii kuomboleza na familia za jamaa na marafiki wa walioangamia, huku nikiwatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa katika ajali hiyo,”alisema waziri Murkomen.
Waziri huyo alisema shughuli za uokoaji zinawahusisha maafisa kutoka asasi mbali mbali za maafisa wa serikali kuu, wale wa serikali za kaunti, viongozi waliochaguliwa, msalaba mwekundu na wasamaria wema.
“Habari zaidi zitatolewa kwa umma. Shughuli za uokoaji zitafuatiwa na uchunguzi kubainisha chanzo cha ajali hiyo.”aliongeza waziri Murkomen.