Zaidi ya watu 30 wamethibitishwa kufariki, baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko katika kijiji cha Kamuchiri eneo la Mai Mahiu, kaunti ya Nakuru.
Afisa mkuu wa polisi anayesimamia eneo la Naivasha Stephen Kirui, amesema watoto 17 ni miongoni mwa waliofariki.
Hata hivyo, idadi hiyo huenda ikaongezeka, huku watu wengi wakiwa hawajulikani waliko, kufuatia kisa hicho kilichotokea Jumatatu asubuhi, wakati watu wengi walikuwa wamelala.
Kisa hicho cha saa kumi alfajiri, kilisababishwa na bwawa lililokaribu kuvunja kingo zake.
Kufuatia ajali hiyo, halmashauri inayosimamia barabara kuu hapa nchini, imefunga sehemu ya barabara kuu ya Mai Mahiu-Suswa-Narok na ile ya Mai Mahiu-Naivasha.