Mwigizaji wa filamu za Nollywood nchini Nigeria Yvonne Jegede ameelezea sababu ya kunyoa nywele, maelezo yaliyowashangaza wengi.
Alichapisha picha ya awali kabla ya kunyoa, baada ya kunyoa na hata video ya wakati akinyolewa.
Msanii huyo kisha aliandadika, “Nimekuwa nikiamini kwamba kusimulia hadithi kwa njia ya ukweli, ni lazima ujitolee kwa jukumu hata kama inamaanisha uondokee unayoyapenda.”
Anasema imani hiyo ndiyo ilimchochea anyoe nywele yake kutokana na kazi anayoendelea kufanya kwenye filamu iitwayo “AJA”.
“Haukuwa uamuzi rahisi lakini kwangu ulistahili ili niingie kabisa kwenye jukumu la uigizaji nililopatiwa ili nilihuishe.” aliendelea kusema Jegede.
Anaitaja kazi hiyo ya “AJA” kuwa ya nguvu na imeandaliwa na Titi Orire. Inasimulia hadithi inayohitaji undani na mabadiliko.
Kando na Jegede, waigizaji wengine walio kwenye filamu hiyo ni pamoja na Rotimi Fakunle, Bianca Ugowanne, Gbohunmi David na msanii mmoja mkubwa wa Nollywood ambaye Jegede ameamua kutomtaja.
“Katika jukumu hili nilijua kwamba ni lazima ningefanya zaidi ya mazungumzo na hisia.” alisema Jegede akiongeza kwamba alihitajika kufanya mabadiliko yanayoonekana ambayo yangemfanya kuingia vizuri kwenye jukumu hilo.
Jegede alisema pia kwamba anafurahia kuigiza pamoja na wenzake tajika katika tasnia ya uigizaji ya Nigeria na anasubiri kwa hamu kuona kazi hiyo itakavyopokelewa na watazamaji.