Miamba wa Tanzania bara Yanga SC ndio mwakilishi pekee wa ukanda wa Afrika Mashariki katika hatua ya makundi kuwania kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga wamefuzu kwa raundi hiyo ya tumu 16 bora kwa mwaka wa pili mtawalia, baada ya kucheza hadi robo fainali mwaka uliopita.
Timu 16 zilizofuzu kwa raundi ya 16 ambayo droo yale itaandaliwa Oktoba 7 zinaongozwa na Misri,Algeria ,Afrika Kusini ,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Morocco mataifa ambayo yametoa vilabu viwili kila moja.
Misri inawakilishwa na Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi pamoja na Pyramids huku Algeria ikiwa na CR Belouizdad na MC Alger.
Afrika Kusini inawakilishwa na Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns huku Morocco ikiwa na AS FAR na Raja Casablanca wakati DRC ikiwa na TP Mazembe na AS Maniema.
Washiriki wengine ni Yanga ya Tanzania,Al Hilal SC ya Sudan, Djoliba AC De Bamako ya Mali,GD Sagrada Esperanca kutoka Angola,Espérance Sportive de Tunis ya Tunisia na Stade d’Abidjan ya Cote d’Ivoire.
Timu mbili bora kutoka kila kundi baada ya mechi sita zitafuzu kwa robo fainali .
Washindi wa kombe hilo watatuzwa shilingi milioni 511 za Kenya .
Al Ahly wanatetea kombe hilo baada ya kutawazwa mabingwa kwa mara ya 12 msimu uliopita walipoibwaga Esperance kwenye fainali.