Wizara ya Kilimo imezindua mpango wa uchunguzi wa udongo kupitia njia ya dijitali kwa lengo la kuhakikisha mipango iliyoimarika na ugavi sawa wa rasilimali.
Hayo yalitangazwa na Waziri wa Kilimo Dkt. Andrew Karanja na Katibu katika Wizara hiyo Dkt. Kiprono Rono, wakati wa hafla ya kuzinduliwa kwa ripoti kuhusu usajili wa wakulima wa mwaka 2023, katika hoteli moja Jijini Nairobi.
Dkt. Karanja alisema usajili wa wakulima ni muhimu kwa kuwa unawezesha wakulima wote popote walipo, wanapata huduma na mipango ya serikali kama vile, mbolea ya bei nafuu, usaidizi wa maafisa wa nyanjani wa kilimo na huduma za fedha.
“Ujumuishaji wa wakulima wote, unasalia kuwa nguzo muhimu wa mpango huu, kuhakikisha hakuna mkulima anatengwa,” alisema Dkt Karanja.
Kulingana naye, usajili wa wakulima na uchunguzi wa udongo, unasaidia pakubwa katika kutoa suluhu maalum kwa kila mkulima, kwa kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo zinazohitajika, mimea inayopendekezwa na kusababisha mavuno yaliyoimarika.
Aidha alisema mpango huu hauwanufaishi tu wakulima, lakini pia unatoa fursa kwa wadau wa kilimo kutenga rasilimali inayohitajika na kuimarisha zoezi la kutathmini miradi ya kilimo.
“Wakulima watanufaika pakubwa kwa kuwa watapokea maelezo kamili kuhusu utumizi wa mbolea, mimea inayostahili na usimamizi bora wa udongo,” alidokeza Waziri huyo.
Aliongeza kuwa, “Mpango huu unaashiria kujitolea kwa serikali kuhakikisha utoshelevu wa chakula, kupunguza kudorora kwa ubora wa udongo na kuimarisha mbinu bora za kilimo kupitia uvumbuzi na ushirikiano”.
Kwa upande wake, Dkt. Kiprono Rono alitoa wito kwa wadau wote wa kilimo kutumia vifaa na takwimu walizo nazo kufanya maamuzi bora katika kuhakikisha ufanisi katika sekta ya kilimo.
Aliwahimiza wakulima kukumbatia majukwaa yaliyopo ya kidijitali, kupata huduma za kilimo zitakazoboresha kilimo chao.
Aliwataka watafiti, maafisa wa nyanjani wa kilimo na wadau katika sekta ya kibinafsi, kushirikiana katika kutekeleza mipango iliyopo ya kufanikisha sekta ya kilimo.