Wizara ya Nishati yamulikwa kwa madai ya ufujaji wa fedha

Tom Mathinji
2 Min Read
Mbunge wa Butere Tindi Mwale.

Kamati ya bunge la taifa kuhusu uhasibu PAC, imeanzisha uchunguzi kubaini jinsi wizara ya nishati ilipokea shilingi milioni 290 zaidi, kutoka Hazina Kuu kwa mradi uliofadhiliwa na wafadhili.

Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za umma iliibua swala hilo, baada ya kubainika kuwa idara ya nishati iliitisha shilingi milioni 90 kwa mradi huo, lakini ikapokea shilingi milioni 378 na hivyo kuwa na shilingi milioni 288 zaidi.

Msimamizi Mkuu wa hesabu za umma  Nancy Gathungu, alitilia shaka maelezo yaliyotolewa na maafisa wa wizara hiyo kwamba mradi huo ulipokea fedha hizo kimakosa na fedha hizo zilikusudiwa kwa mradi mwingine.

Wanachama wa kamati hiyo walipokuwa wakikagua matumizi ya fedha katika idara ya nishati katika kipindi kilichokamilika Juni 30,2024, walitaja tukio hilo kuwa la kutiliwa shaka.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Tindi Mwale ambaye ni mbunge wa Butere, alimtaka katibu katika wizara ya nishati  Alex Wachira  kuelezea iwapo ni jambo la kawaida kwa makosa kama hayo kutokea serikalini.

Hata hivyo, Wachira alikuwa na wakati mgumu, huku majibu yake yakikosa kuwaridhisha wabunge hao.

“Swali tunalouliza ni je, fedha hizo zilirejeshwa au zilitoweka kutoka hazina kuu?”, aliuliza mbunge wa Soy David Kiplagat asked.

Aidha kamati hiyo iliagiza ikabidhiwe stakabadhi za makubaliano kati ya hazina kuu na benki ya dunia kuhusu mradi huo.

Maafisa kutoka hazina kuu waliohudhuria mkutano huo, walisema makosa ya kutoa fedha zaidi ya zilizohitajika si ya kawaida.

TAGGED:
Share This Article