Wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi imesema kwamba imejitolea kikamilifu kushirikiana na maafisa wa usalama wanaochunguza visa vya mauaji ya wanawake kuhakikisha haki inatendekea.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Waziri Aisha Jumwa, wizara hiyo inahimiza maafisa wa usalama kutekeleza uchunguzi wa kina na yeyote atakayepatikana na hatia achukuliwe hatua kali za kisheria.
Jumwa anasema visa vilivyoshuhudiwa vya wanawake kuuawa kwenye vyumba vya kukodisha ni dhihirisho kwamba ni lazima hatua zichukuliwe kutokomeza dhuluma dhidi ya wanawake katika jamii.
Alizungumzia pia wanaolaumu na kuaibisha waathiriwa wa visa hivyo akisema kuendelea kufanya hivyo ni kuwadhulumu kwa mara nyingine.
Huku akitoa ujumbe wa pole kwa familia za waathiriwa Waziri Jumwa alifafanua kwamba wizara yake imejitolea kuunga mkono watu wa jinsia zote huku ikihimiza utamaduni wa heshima usawa na usalama katika jamii.
Taarifa hii ya waziri Aisha Jumwa inajiri kufuatia visa mbali mbali vya wanawake kupoteza maisha mikononi mwa wanaume wanaojisingizia kuwa wateja wa ngono.
Starlet Wahu aliuawa na jamaa kwa jina John Matara ambaye baadaye alikamatwa na maafisa wa polisi. Wanawake wengi wamejitokeza kudai kudhulumiwa na mshukiwa huyo.
Jumapili Januari 14, 2024, mwili wa mwanamke mwingine ulipatikana ukiwa bila kichwa katika eneo la Roysambu. Ametambuliwa kama Rita Waeni Muendo.