Wizara ya Afya leo Jumatatu imezindua sensa ya vituo vya afya kote nchini.
Wizara inasema sensa hiyo itakayofanywa kwa muda wa wiki mbili itakuwa muhimu katika kuufanyia mabadailiko mfumo wa afya nchini.
Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni anasema wizara hiyo, ikiongozwa na maono imara, imechukua hatua kubwa kuelekea kutoa kipaumbele kwa afya ya umma ya msingi.
“Mabadiliko haya ya kimkakati, ambayo yamejikita kwenye wajibu wa wahamasishaji afya ya jamii mashinani, yanalenga kuongeza shabaha yetu kuelekea kuzuia na kuhamasisha, kuziwezesha jamii na kukuza mtazamo tekelezi wa afya unaovuka mipaka ya hali ya kawaida ya utoaji matibabu,” alisema Muthoni wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika uwanja wa wizara hiyo.
“Zoezi hili linalenga kuhakikisha upatikanaji wa afya kwa wote ambayo ni maono ya serikali kama ilivyoelezwa kwenye ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi kuanzia chini kuelekea juu.”
Hususan, katibu huyo alisema zoezi hilo kadhalika linakusudia kupata uelewa wa vituo vya afya vilivyopo nchini, rasilimali zinazomilikiwa na vituo hivyo na huduma zinazotolewa ili kutoa mwelekeo wa kubuniwa kwa sera unaoongozwa na hali halisi, upangaji mzuri na uwekaji wa programu katika sekta ya afya kwa kutafakari ili kuafikia upatikanaji wa afya kwa wote unaooongozwa na data.
Kadhalika linanuia kubaini uwezo wa vituo vya afya kwa mantiki ya wahudumu wa afya siyo tu walio na ujuzi unaohitajika bali pia walio na uelewa wa kisasa na ambao wako tayari kuangazia mahitaji yanayobadilika ya watu mbalimbali.
Zoezi lenyewe litaendeshwa na watafiti wasaidizi 500 watakaoongozwa na maafisa 47 wa kiufundi wa wizara na waratibu 10 wa kikanda.
Data za vituo vya afya zaidi ya 15,000 vya serikali, vya kidini na vya kibinafsi zitakusanywa wakati wa zoezi hilo.
Katibu Muthoni alisisitiza nia ya serikali kuboresha utoaji huduma za afya kote nchini.