Wizara ya Afya na Baraza la Magavana wamefafanua kuhusu mpango wa kitaifa wa vifaa vya afya.
Hatua hii inafuatia makala yaliyochapishwa na gazeti moja la humu nchini kuhusu mpango huo.
Katika kusuluhisha kumalizika kwa muda wa utekelezaji wa mpango huo Disemba 2023, serikali imezindua mkakati mpya wa kuuendeleza kutokana na mafanikio ya mpango huo.
Mkakati huo uliundwa kufuatia maazimio ya kongamano la 10 lisilo la kawaida kati ya serikali za kaunti na serikali ya kitaifa Disemba 18, 2023.
Unahusisha mfumo wa kiwango kamili cha ada itakayotozwa kwa ukarabati wa vifaa unaokubalia wauzaji kuleta vifaa hivyo, kuvitunza na kuviboresha katika hospitali za kaunti bila gharama zaidi.
Mfumo huu tofauti na mfumo wa kukodisha vifaa ulioripotiwa, unahamisha jukumu la kifedha hadi kwa muuza vifaa. Unawezesha kaunti kuangazia utunzaji wa wagonjwa zikihakikisha pia uwepo wa vifaa vya kisasa zaidi.
Baraza la magavana na wizara ya afya zimesisitiza kwamba mchakato wazi wa utoaji zabuni ulitekelezwa na wakaafikia wauzaji saba Oktoba mwaka 2024.
Mapango huo mpya umeundwa kwa namna itakayouwezesha kuwa wa kufanikiwa, wazi na endelevu.
Lengo kulingana na aasasi hizo mbili za serikali ni kuimarisha utoaji huduma za afya kote nchini. Zimejitolea kuunga mkono huduma za afya kupitia mifumo shirikishi na yenye uwajibikaji.