Wito watolewa wa kuongezwa ufadhili kwa sekretarieti ya EAC

Tom Mathinji
2 Min Read

Makarani wa mabunge katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC wametoa wito wa kuongezwa ufadhili kwa sekretarieti ya jumuiya hiyo. 

Wito huo ulioongozwa na Naibu Karani wa Bunge la Taifa la Kenya Jeremiah Ndombi, aliyetaka mataifa wanachama kuendelea kuunga mkono Bunge la Afrika Mashariki, EALA.

“Sekretarieti ya bunge hili la EALA Kwa sasa inakumbwa na changamoto. Inahitaji usaidizi wa kifedha na nguvukazi ili kuhudumia kanda hii kikamilifu,” alisema Naibu huyo wa Karani wa Bunge la Taifa la kenya.

“Tusichoke kuunga mkono Sekretarieti ya Bunge la Afrika Mashariki,” aliongeza Ndombi.

Ndombi aliyasema hayo wakati wa mkutano wa makarani wa mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, ulioandaliwa katika hoteli moja jijini Nairobi.

Naibu Karani wa bunge la EALA John Mutega, alifahamisha mkutano huo kuwa wafanyakazi wa bunge hilo hawajalipwa mshahara wa mwezi Oktoba.

Ndombi alielezea maono ya kuwa na taifa moja la Afrika Mashariki, akisisitiza jukumu la afisi ya spika wa EAC kuafikia hayo.

“Ningependa kuona Jumuiya moja ya Afrika Mashariki iliyo na wimbo mmoja wa taifa,” alisema Ndombi.

Akiwakilisha bunge la Senate la Kenya, Naibu Karani wa Senate Mohamed Ali, alisema ni heshima kubwa kwa Kenya kuandaa mkutano wa maspika wa Afrika Mashariki .

Mkutano ujao wa maspika wa Afrika Mashariki, utawaleta pamoja viongozi kutoka mabunge ya taifa, Seneti na EALA, kujadili maswala yanayoathiri utangamano wa Afrika Mashariki.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article