Serikali za kaunti zimetakiwa kufufa programu za kudhibiti ugonjwa wa malaria zilizokwama kutokana na mlipuko wa janga la virusi vya korona nchini.
Shirika la kimataifa la “Malaria No More UK” limelalama kuwa programuu ambazo zilikuwa zimewekwa kudhibiti ugonjwa huo nchini zimekwama, hatua ambayo imesababisha ongezeko la wagonjwa katika hospitali nyingi kote nchini.
Rodah Igweta ni Mkurugenzi wa Afrika wa shirika la Malaria No More UK. Amesema kasi ya kampeni za kuzuia ugonjwa wa malaria na usambazaji wa rasilimali za kutokomeza ugonjwa huo ilipungua wakati shabaha ilipoelekezwa kwa janga la virusi vya korona.
Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa ugatuzi uliomalizika mjini Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu, Igweta alisema hatua za kuzuia ugonjwa huo ni rahisi na zinazoweza kufikiwa katika viwango vya wadi ikizingatiwa kwamba afya imegatuliwa.