Wasanii wa muziki nchini Tanzania Billnass na Mbosso wametozwa faini ya shilingi milioni 3 kila mmoja na kufungiwa kwa muda wa miezi mitatu.
Adhabu hiyo kutoka kwa Baraza la Sanaa la Taifa – BASATA imechochewa na kuhusika kwa wasanii hao kwa wimbo wa msanii mwenza Whozu kwa jina “Ameyatimba”.
BASATA inataja maudhui ya wimbo huo kuwa kinyume na maadili.
Marufuku dhidi yao inaanza Nobemba 4, 2023.
Whozu alitakiwa kuondoa video ya wimbo huo kwenye majukwaa yote mitandaoni, akatozwa faini ya shilingi milioni 3 na kufungiwa kujihusisha na kazi za sanaa ya muziki kwa muda wa miezi 6.
BASATA inasema picha na maneno kwenye wimbo huo uliochapishwa Novemba 2, 2023, unakiuka kanuni za maadili kwa sababu ya maneno na vitendo vya matusi kinyume na Kanuni nambari 25 sehemu ya 6 (j) na vitendo ya unyanyasaji, ukatili na udhalilishaji wa utu wa mwanamke kinyume na Kanuni nambari 25 sehemu ya 6 (f).
BASATA ilisema pia kwamba msanii Whozu ameonywa mara mbili na kutozwa faini mara moja kwa kukiuka maadili lakini ameendelea kufanya hivyo.
Baraza hilo linasisitiza kwamba kila msanii nchini Tanzania ni lazima azingatie maadili ya kijamii jinsi ilivyoratibiwa kwenye mwongozo wa maadili.
Wasanii hao wamehimizwa kujifahamisha kuhusu maadili kwenye mwongozo huo ambao unapatikana kwenye tovuti www.basata.go.tz.