Wetang’ula ateuliwa mwanachama wa jopo la maspika wa mabunge Afrika

Marion Bosire
2 Min Read

Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula ameteuliwa mwanachama wa jopo la ushauri la shirikisho la maspika na marais wa mabunge barani Afrika.

Uteuzi huo ulifanyika jana Jumamosi katika mkutano wa pili wa shirikisho hilo jijini Accra, nchini Ghana, ambapo wanachama walijadili kuhusu katiba ya shirikisho hilo na kuiidhinisha.

Wetang’ula ambaye anajiunga na viongozi wengine mashuhuri kwenye jopo hilo lililojukumiwa kuongoza katika masuala ya sera na mwelekeo aliwakilishwa kwenye mkutano huo na mbunge wa Ugenya David Ochieng.

Spika wa bunge la Ghana Alban Sumana Kingsford Bagbin aliongoza mkutano huo uliohudhuriwa na maspika zaidi ya 10, manaibu spika wapatao 20 .

Shirikisho hilo lilibuniwa mwaka 2020, kwa lengo la kuunganisha maspika wa mabunge ya bara Afrika ili kushughulikia changamoto zinazokabili bara hili.

Wanachama walikubaliana kwamba makao makuu ya shirikisho la maspika na marais wa mabunge barani Afrika yatakuwa jijini Abuja nchini Nigeria.

Katiba ya shirikisho hilo imezungumzia makundi kadhaa chini yake kama vile, mkutano mkuu, kamati kuu na jopo la ushauri.

Jopo la ushauri litakuwa na wanachama hadi 10, watano wanaohudumu na watano waliokuwa wakihudumu awali kama maspika.

Huku akikubali uteuzi huo, Ochieng alisema kwamba Wetangula anatosha kuhudumu katika jopo hilo kutokana na tajriba yake ya muda mrefu kama mbunge.

Share This Article