Viongozi wa eneo la Magharibi mwa nchi wameanzisha shinikizo za umoja wa kisiasa wanapotafuta kuwa na ushawishi na hatimaye kuweka mmoja wao mbele kuwania urais mwaka 2032.
Wakizungumza kwenye mazishi ya Mzee Peter Nasong’o Nabwera katika eneo bunge la Lugari kaunti ya Kakamega, viongozi wakuu wa kisiasa katika eneo hilo walisisitiza haja ya umoja wa jamii ya Luhya.
Kulingana nao, umoja wao na wingi wao utageuka kuwa nguvu kuu ya kisiasa katika upigaji kura nchini.
Gavana wa kaunti ya Kakamega Fernandes Barasa, alilalamika kwamba jamii hiyo haijaweza kutumia wingi wa watu wake kuafikia ufanisi katika uchaguzi.
“Umoja ndio njia ya pekee ya kupata heshima na kupata nafasi yetu faafu katika siasa za kitaifa.” aliongeza Barasa huku akihimiza viongozi wahamasishe wapiga kura.
Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula aliibuka kuwa mwaniaji anayekubalika na wote kwa urais mwaka 2032, ambapo viongozi waliahidi kumuunga mkono wakitaja uongozi wake kuwa matumaini kwa maazimio ya eneo hilo.
Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, alihimiza viongozi wenzake kuunga mkono viongozi wakuu badala ya kuwahujumu ili wawaongoze katika kuafikia ushindi.
Wetang’ula, mwanasiasa aliye na uzoefu wa zaidi ya miongo mitatu bungeni amehusishwa na hayati Mwai Kibaki, ambaye kazi yake ya muda mrefu kama mbunge ilikamilika katika urais uliofanikiwa.
Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah alimsifia sana Wetang’ula, akidhihirisha imani katika uwezo wake wa kuinuka na kuingia katika afisi kubwa zaidi humu nchini.
Viongozi walisisitiza pia haja ya kumuunga mkono Rais William Ruto. Gavana Barasa, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ODM Kakamega, alisema kwamba kumuunga mkono Rais kutaweka eneo hilo pazuri kwa ajili ya siku zijazo.
Wetang’ula kwa upande wake alisisitiza umuhimu wa mipangilio mizuri akionya dhidi ya matumizi ya mikutano ya mazishi kama majukwaa ya kujadili mikakati.
Alihimiza kupangwa kwa mikutano ya kupanga mustakabali wa eneo la magharibi.
Spika huyo alihimiza pia usajili wa wapiga kura katika eneo hilo akizitaka kaunti kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao kupitia kwa kusajili wapiga kura wengi.
Marehemu Mzee Peter Nasong’o Nabwera ni kakake aliyekuwa waziri Burudi Nabwera na mjomba wa mbunge wa Lugari Nabii Daraja Nabwera.