Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula, amewaarifu wabunge na wananchi kuhusiana na taarifa ya Rais William Ruto kuhusu mswada wa fedha wa mwaka 2024.
Katika arifa hiyo, Spika huyo amewasilisha taarifa hiyo kwa kamati ya bunge la kitaifa kuhusu fedha na mipango.
Amesema kamati hiyo inatarajiwa kuanza kwa haraka kuzingatia taarifa hiyo ya Rais, kuzingatia yaliyomo na mapendekezo yake, na kuwasilisha ripoti bungeni katika kikao kijacho cha kawaida baada ya bunge kurejelea vikao vyake.
Wetang’ula amemuagiza karani wa bunge kusambaza taarifa hiyo kwa wabunge wote na kufanikisha utekelezaji wa shughuli hiyo.
Hayo yamejiri baada ya Rais William Ruto Jumatano wiki hii kutangaza kuwa hatatia saini kuwa sheria mswada wa fedha wa mwaka 2024, baada ya maandamano kushuhudiwa kote nchini siku ya Jumanne kupinga mswada huo.
Rais alisema alichukua hatua hiyo kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Bunge lilikwenda mapumzikoni Jumatano na litarejelea vikao vyake vya kawaida Jumanne, Julai 23 mwaka huu.