Wenyeji Ufaransa walifungua makala ya mwaka huu ya kombe la dunia katika raga ya wachezaji 15 kila upande kwa ushindi wa pointi 27-13 dhidi ya Newzealand Ijumaa usiku uwanjani Stade de France mjini Saint Dennis.
Newzealand maarufu kama All Blacks walichukua uongozi wa mapema kupitia kwa tries mbili za Mark Telea kunako dakika ya 2 naye Richie Mo’unga akafunga penati ya dakika ya 25.
Ufaransa waliongoza kipindi cha kwanza alama 9 kwa 8 baada ya Thomas Ramos kufunga penati tatu.
Wenyeji waliongeza makali kipindi cha pili Damian Penaud na Melvyn Jaminet wakifunga tries moja kila mmoja kwa Ufaransa naye Ramos akafunga conversion kabla ya kutanua uongozi kwa kupachika penati mbili.
Waakilishi wa Afrika,Namibia watashuka uwanjani Jumamosi Septemba 9 kwa mchuano mwingine wa kundi A ,kabla ya Ireland kuvaana na Romania kundini B huku Australia wakipimana nguvu na Georgia katika kundi C kisha Uingereza wachuane na Argentina katika kundi D.
Mechi za makundi zitakamilika Oktoba 8 kabla ya kupisha robo fainali kati ya tarehe 14 Oktoba na 15 na semi fainali ichezwe tarehe 20 na 21 na hatimaye fainali isakatwe Oktoba 28.