Wenye magari kutozwa ushuru wa asilimia 2.5

Martin Mwanje
2 Min Read

Ni kilio kwa wanaomilikia magari nchini baada ya serikali kupendekeza kuwa watakuwa wanalipa ushuru wa asilimia 2.5 kwa mwaka. 

Hatua hiyo ni njia moja tatanishi ambayo serikali inalenga kutumia kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kulipa madeni na kufadhili miradi mbalimbali nchini.

“Bwana Spika, ili kupanua wigo wa walipa ushuru na kuifanya nchi yetu kujitegemea, napendekeza kuanzishwa kwa ushuru wa magari utakaotozwa kwa mwaka kwa kiwango cha asilimia 2.5 cha thamani ya gari husika huku kiwango cha chini cha ushuru huo kikiwa shilingi 5,000 kwa mwaka,” alisema Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u wakati akisoma bajeti bungeni jana Alhamisi.

Wakenya wamepinga vikali kutozwa kwa ushuru huo wakisema hatua hiyo itakuwa sawia na kuwatoza ushuru mara mbili.

Pingamizi dhidi ya ushuru huo zilikolea wakati washikadau mbalimbali walipofika mbele ya kamati ya fbunge ya fedha na mipango ya kitaifa inayoongozwa na mbunge wa Molo Kuria Kimani ili kutoa maoni yao kuhusiana na Mswada wa Fedha 2024.

Mswada huo ulipendekeza kutozwa kwa ushuru wa asilimia 2.5 kwenye magari ila kiwango cha chini kilipendekezwa kuwa shilingi 5,000 na cha juu zaidi shilingi 100,000, hatua ambayo karibu wadau wote walipinga vikali.

Katika bajeti iliyosomwa jana Alhamisi, kiwango cha juu cha shilingi laki moja kimeondolewa, ikiwa na maana kwamba baadhi ya Wakenya wenye magari ya kifahari huenda wakalipa ushuru wa hadi shilingi nusu milioni kwa mwaka.

Hatima ya ushuru huo itajulikana bayana wakati kamati ya bunge ya fedha na mipango ya kitaifa itakapowasilisha mswada huo bungeni wiki ijayo.

 

Website |  + posts
Share This Article