Weasel asema Abba atajifunza kutokana na makosa yake

Makosa hayo kulingana na Weasel ni kufichua anachougua babake na hulka yake ya unywaji pombe kupita kiasi.

Marion Bosire
1 Min Read

Douglas Mayanja mwanamuziki wa Uganda maarufu kama Weasel Manizo, ambaye ni kaka mdogo wa Jose Chameleone amezungumzia lawama za mpwa wake Abba Marcus dhidi ya babake Jose Chameleone.

Weasel anaonya mtoto huyo akome kumshambulia babake mitandaoni la sivyo masaibu sawa na ya babake yatamfika.

Onyo la Weasel linajiri siku kadhaa baada ya Abba, ambaye ndiye mtoto mkubwa wa Chameleone, kujitokeza mitandaoni kuzungumzia masaibu ya babake mzazi.

Kabla ya hapo, familia ya Chameleone haikuwa imefichua anachougua hata baada yake kulazwa hospitalini mara kadhaa tangu mwaka jana.

Abba alisema babake anaugua ugonjwa wa Kongosho unaotokana na unywaji pombe kiholela na kupita kiasi.

Hata ingawa Abba alifafanua kwamba tangazo lake halikulenga kumchafulia babake jina, watu wa familia ya babake wanahisi kwamba alimdhalilisha.

Marcus alisema unywaji pombe ndio umesababisha babake ambaye ni mwanamuziki maarufu apoteze uzani wa mwili huku akinyoshea nyanyake na babu yake kidole cha lawama.

Kulingana naye, walistahili kuwajibika zaidi kudhibiti ulevi wa Jose Chameleone lakini wanachofanya ni kufurahia tu mapato yake.

Abba amesema kwamba ufichuzi wake umemfanya babake ambaye yuko Marekani kwa matibabu amnyamazie kwani aliacha kuchukua simu zake.

Weasel, anaonekana kughadhabishwa na matamshi ya mpwa wake lakini anatumai kwamba hatimaye ataelewa shida za babake mzazi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *