Waziri Owalo azindua mtandao wa Wi-Fi Ukunda

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Digitali Eliud Owalo amezindua mtandao wa Wi-Fi katika soko la Ukunda, eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale.

Mpango huo unaambatana na ajenda ya dijitali ya serikali ya Kenya kwanza chini ya uongozi wa Rais William Ruto.

Waziri aliandamana na Gavana wa Kwale Fatuma Achani wakati wa uzinduzi huo.

Owalo alisema alivutiwa na kujitolea kwa wanabiashara wa eneo hilo kukumbatia teknolojia ya kidijitali na biashara ya mtandaoni kupanua wigo wa biashara zao hata nje ya nchi.

Kulingana naye, wizara yake inaongeza viwango vya ujuzi wa kidijitali na mtandao wa Wi-Fi kote nchini.

Alisema serikali ya Rais Ruto hivi karibuni itatoa simu za bei nafuu zilizoundwa nchini Kenya na ambazo bei ya rejareja itakuwa dola 40.

Aliishukuru serikali ya kaunti ya Kwale kwa kuonyesha nia ya kushirikiana na serikali kuu katika mpango kwa kidijitali.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa Wi-Fi ni naibu Gavana wa kaunti ya Kwale Josephat Kombo, seneta mteule Miraj Abdilahi, mbunge wa Msambweni Faisal Bader na naibu kamishna wa Msambweni Bwana Kipkech.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *